maambukizi ya ukimwi yatishia uhai kwa watoto
Bagamoyo.Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameelezwa kuwa tishio na asilimia 50 ya watoto wanaozaliwa na virusi vya ugonjwa huo hupoteza maisha ndani ya miaka miwili tangu kuzaliwa wasipopatiwa dawa za kupunguza makali ya virusi (ARV).
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la
kiserikali la EGPAF linalojishughulisha na harakati za kutokomeza
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Dk Jeroen Van’t Pad
Bosch, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyolenga
kuwajengea uwezo wa kuandika habari zihusuzo maambukizi ya Ukimwi toka
kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mkurugenzi huyo alisema miongoni mwa wanawake
wajawazito 100 wenye virusi vya Ukimwi wasipopatiwa dawa, watoto
wanaozaliwa asilimia 80 hupoteza maisha ndani ya miaka mitano na vifo
vingi vinatokana na kinamama hao kutotii masharti wanayopewa wakati wa
kliniki na baada ya kujifungua.
Alisema waandishi wa habari wana kila sababu ya
kujikita katika kuandika habari za Ukimwi ili wananchi waone umuhimu wa
kupima na kutumia dawa mapema.
Alisema licha ya elimu hiyo kutolewa kila mara, bado kuna watu hawaoni umuhimu wa kupima mapema.
Naye mtaalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Grace Dennis alisema kiwango cha maambukizi kwa watoto nchini
kimefikia asilimia 15.7 kwa takwimu za mwaka 2013, na kwa sasa Serikali
imedhamiria kupunguza maambukizi hayo hadi kufikia asilimia nne ifikapo
mwaka kesho.
Alisema changamoto iliyopo ni kwa wajawazito
wanaojifungulia nyumbani kukosa nafasi ya kupima ili wapatiwe huduma
zinazostahili mapema, ikiwamo ya dawa za ARV na huduma za uzazi salama
ambazo wengi wao huzikosa.
No comments:
Post a Comment